WATOTO WA MAMA NTILIE....

Fatilia uchambuzi mzuri kwa maandishi pamoja na full video bila wasi wasi Sasa karibu tuanze

UCHAMBUZI  WA FASIHI SIMULIZI
WATOTO WA MAMA NTILIYE
KIPENGELE  CHA  FANI: 
1.     mwanafunzi atatakiwa kujibu maswali yatayohusiana na kipengele cha fani, 
2.     rejea vipengele vya fani katika vitabu mbalimbali
MWANDISHI:         EMMANUEL MBOGO
WACHAPISHAJI: HEKO PUBLISHERS
MWAKA: 2002

JINA LA KITABU
Jina la kitabu WATOTO WA MAMA NTILIE limesadifu yaliyomo ndani ya kitabu, kinaeleza kuhusu maisha ya watoto wa mama ntilie. Maisha ya dhiki, umaskini uliokithiri, maisha yasiyo ya faraja yaliyokosa malezi bora, chakula bora, elimu, huduma ya afya nk. Jina la kitabu linaakisi yaliyomo ndani ya kitabu na katika jamii yetu ya leo kwani akina mama wengi hawana kazi nzuri za kuwaingizia kipato kikubwa na bado wanategemewa katika malezi. Mwandishi ametumia jina hili ili kibua kero na matatizo yaliyoko katika jamii.
UTANGULIZI WA KITABU
Riwaya ya Watoto wa Mama N’tilie ni riwaya ambayo inasadifu maisha ya Mtanzania wa leo. Inaangazia suala la umaskini  na hali ngumu ya maisha, wimbi la watoto wa mitaani, masuala ya uhalifu wizi na ujambazi, malezi nk. Mwandishi Mbogo amejitahidi sana. Pia katika fani ametumia muundo na mtindo wenye kuwavutia wasomaji pia kawaumba wahusika wake kwa usadifu wa hali ya juu huku mandhari yake ikiwa ni halisi inayosawiri maisha ya Tanzania.
FANI
MUUNDO
Muundo uliotawala katika riwaya hii ni muundo wa rukia au rejea. Mfano sura ya tatu mwandishi anatuelezea juu ya safari ya Mama ntilie kwenda matombo uk.34. Lakini anaacha kisa hicho ndani ya sura hiyohiyo anaanza kutuelezea juu ya kuzaliwa kwa watoto Kurwa na Doto na asili yao. Pia uk.80 mwandishi anatudokeza juu ya safari ya kwenda kwa Musa na hatuoneshi hatma ya safari yake bali anarukia kisa kingine na kuanza kutuelezea juu ya Zita kupandwa na kichaa uk.81. Vilevile uk.85-86 anatusimulia juu ya safari ya Mama Zita na Zenabu kuelekea hospitali kumwona Zita lakini hatuoneshi hatma ya safari yao bali anarukia kisa kingine na kuturudisha nyumbani kwa Mzee Lomolomo na jinsi anavyofakamia pombe alafu anaturudisha tena kutuambia juu ya kifo cha Zita hospitalini Muhimbili.
Mwandishi amegawa visa na matukio katika sura tano. Sura hizi zimejengwa katika muundo unaotegemeana ili kukamilisha kilele cha masimulizi.
MTINDO
Mtindo aliotumia mwandishi ni wa masimulizi ya mjazo au lugha ya nathari ameeleza visa mwenyewe na vingine wahusika wamevielezea. Pia ametumia mitindo kadha wa kadha. Mfano;
Matumizi ya nafsi
Nafsi ya tatu wingi na umoja
Uk.15 “Peter aliokota kipande cha muhogo” “alisafisha kipande cha muhogo”
Uk.27 “walisaidiana wakaubeba” uk.26 “watu walisongamana walisukumana…..”.
Kwa kiasi kikubwa matumizi ya nafsi ya tatu ndiyo yaliyotawala.
Nafsi ya kwanza umoja na wingi
Uk.58 “nitasema nitasema!”
Uk.58 “njoo tuongee”
Uk.56 “twende tule”
            Matumizi ya nafsi ya pili au dayalojia
Uk.89 pale Mama ntilie alipokumbuka majibizano yake na Zita.
MAMA NTILIE: na hiyo nguo namna gani? Mbona chafu hivyo na leo ndio kwanza
                             Jumanne.
PETER: mbwa Mama……
ZITA: amenikwaruza kidogo na makucha yake.        
            Matumizi ya tanzu nyingine za kifasihi, mfano wimbo
Uk.78 “Jua ni moto
             Tena ni mwangaza
              Wa  Dunia
              Nadina yoo
              Nadina mama
              Tumwombe Mungu Baba”
Uk.10 wimbo alouimba mzee Lomolomo.
            “Kuleni nae
              Hata bangi vuteni nae
              Lakini ni kazi bure
              Mwenzenu nimezaa naye
              Pepepe kijani cha mbaazi
              Kijaluba na msondo
              Kiboko yao”.      
Hivyo mwandishi ametumia mitindo hiyo ili kutomchosha msomaji mfano wimbo unamburudisha msomaji, majibizano yanavuta umakini zaidi na matumizi ya nafsi mbalimbali.
MATUMIZI YA LUGHA
Riwaya ya Watoto wa Mama Ntilie imetumia lugha rahisi, fasaha na inayoeleweka kwa wasomaji. Kuna matumizi ya lugha ya kiingereza mfano. Uk.36 “chloroquine”, “Rosewine na Queen Elizabeth”, Uk.83 “faster faster mama” uk.1 “landrover”. Pia kuna matumizi ya lugha ya miitaani uk.41 “kudeku…..”
Matumizi ya tamathali za semi
Tashibiha
uk.10 “mdomo wake ulio kaa kama bakuli la pombe”
Uk.12 “mama ntilie alikaa kama kapigwa na radi”
Uk.15 “miguu kama ya mamba”
Uk.46 “aliinamisha shingo nayo ikapinda kama mforosadi” “kichwa kama stafeli”
Uk.40. “kitovu chake kama jicho chongo”
Uk.23 “Kurwa aliruka nyuma kama Chui”
Uk.45 “akaruka kama Paa”
            Tashihisi
Uk. 10 “mabega yenyewe tayari yalikuwa yamechongwa kwa pombe ya gongo                    
              Yameangalia juu karibu yakutane na masikio”
Uk.17 “aliziona nywele za kipilipili za Musa ngumu kama katani hazijaonja maji wala
             sabuni”
Uk.19 “ moshi wenye harufu ya kuudhi ulilelea hewani na kumlaki mtoto Peter.”
Uk.35 “…… visogo vitatu vilikata kona na kupotea”
Uk.46 “koo lilimsaliti”
Uk.40 “miguuni raba zinazocheka kwa huzuni”
Uk.46 “mlango ule wa kuungwa na gundi ulitika labeka”
Sitiari
Uk.10 “Nyama nyie”
Uk.86 “…… wakatembea mwendo wa Farasi”
Ritifaa
Uk.38 “Mama? Mama yuko wapi, Baba yuko wapi? Mapenzi yao yako wapi?”
Uk.92 “Zita! Zita! Zita! Zita umekwenda! Umenitoroka, Zita mwanangu”
Uk.93 “Baba! Baba watoto? Mwenzangu! Ee! Amka, simama! Usiniachie tanzia hii peke
             Yangu”
Tafsida
Uk.91 “haja kubwa”
Matumizi ya mbinu nyingine za kisanaa.
Onomatopea /tanakali sauti
Uk.5 “….. aliupinda mgongo kwa mbele akausikia unalia ka-ka-ka-ka, alitema mate tena
           Phuuuu”
Uk.11 “alikohoa ukho! okho!”
Uk.19 “…. Kwa kupiga chafya mbili au tatu Tcha! Tcha! Tcha!”
Uk.50 “Bwee! Bwee! Bwee! Mbwa ….”
Uk.50 “Hali … vicheko Woo! Woo! Weee! Weee! Heheheee! Leooo!”
Takriri
Uk.12 “twende! Twende! Nakuwacha nakauwacha!”
Uk.58 “ Nivione! Nivione! Nivione vya kazi gani!”
Uk.60 “ Nipishe! Nipishe! Nipishe!
Uk.61 “kukurukakara, kukurukakara,kukurkakara”
Uk.91 “ Baba! Baba! amka Baba”
Mjalizo
Uk. 40 “… akapata pesa, akala, akashiba”
            Mdokezo
Uk.58 “usiseme hivyo! Unasikia ee! Usi……”
Uk.71  mara akaanza kuimba tena uleule wimbo wake wa  “siwezi kuuwa mtu
            mama”
Uk.73 “lakini…….”
Uk.79 “ alikumbuka jaa laa jiji na ………”
Nidaa
Uk.44 “ Oh! Mungu wangu!”
Uk.91 “ Mama wee!”
Uk.90 “Hamadi! Mtume!”
Matumizi ya semi
Nahau
Uk.43 “…. Kupiga usingizi”
Methali
Uk.34 “ kamba hukatikia pembamba”
Uk. 69 “fadhila za Punda”
Misemo
Uk.35 “ mtu wa maji” – mlevi.
Uk.13 “kwake pombe ya mataputapu na gongo alivifanya dini”.
Matumizi ya taswira
Taswira mwonekano mfano
Uk.1 “ Mbwa huyu mweusi mwenye mkia mweupe, alionekana akitembea mwendo wa polepole. Ulimi wake mrefu ulionekana ukidondoka mate ya utelezi” hii inatufanya tupate picha halisi ya jinsi Mbwa huyo alivyo kupitia maneno ya msanii”.
Uk.5 “….. hatua tatu mbele yake Sufuria, Vikombe na Sahani chafu zilizagaa pale nje zikimtazama. Akawaona nzi wakitembea na kurukaruka juu ya vyombo vichafu.
Uk.10 “ mabega yenyewe tayari yalikuwa yamechonngoka kwa pombe ya gongo yameangalia juu karibu yakutane na masikio.”
Uk.69 “Zenabu alibaki pale mlangoni kavaa gauni aina ya shifti, kitambaa cha Hariri”
Taswira hisi
Uk.91 “ Mzee Lomolomo alilala mdomo wazi Nzi wakubwa wa kijani kibichi wamejaa tele mdomoni mwake”. Hii inamfanya msomaji ajisikie kinyaa kutokana na hali hiyo ya Mzee Lomolomo anaposema nzi wa kijani kibichi, kwani hao ni nzi wanaokaa sana chooni na kwenye uchafu.
WAHUSIKA
Mama Ntilie
Ni mama mzazi wa Peter na ZitaNi mke wa Mzee LomolomoMlezi mzuri wa familiaNi mvumilivu sanaAna hurumaNi mchapakazi na anayejitumaAna hali ngumu kimaisha
Mzee Lomolomo
Ni mme wa mama ntilieBaba wa Peter na ZitaMleviMvivuSi mlezi bora hajali familiaAnakufa kwa sababu ya kunywa sana pombe
Peter
Mtoto wa mama ntilieAnakosa elimu kwa sababu ya umaskiniAna bidii na mchapakaziAna hurumaAnafungwa jela sababu ya kufanya biashara haramu ya madawa ya kulevya
Zita
Mtoto wa kike wa mama ntilieAnakosa elimu sababu ya umaskiniNi mchapakaziAnagombana na Kurwa hakupenda aje kwao, roho mbayaAnakufa kwa ugonjwa wa kichaa cha mbwa
Doto
Ni mtoto yatimaMtoto wa mtaaniDoto anauawa baada ya kujiingiza katika uhalifu wa wiziNi mgomvi na katili
Kurwa
Ni ndugu yake DotoAnaishi mtaaniNi yatimaAna hurumaAna nguvu na jasiriNi mchapakaziAnaishia jela kwa sababu ya makosa ya Musa na Peter
Zenabu
Ni jirani wa Mama ntilieAna hurumaMfanyakazi wa baaAlimsaidia kurwa kumpeleka hospitali baada ya kupandwa na kichaa.
Musa
Ni mtoto aliyekosa elimu baada ya kukosa sare na adaAlikosa malezi mazuri ya wazaziMhalifu, anafanya biashara haramu za madawa ya kulevyaAna tamaa ya pesaNi rafiki mbaya kwani alimshauri Peter kuuza madawa ya kulevya
Mwalimu Chikoya
Ni mwalimu  wa akina Peter na ZitaAliwafukuza Peter na Zita shule sababu ya kukosa adaSi mwalimu mzuri
MANDHARI
Mandhari iliyotumika katika riwaya hii ni mandhari ya jiji la Dar es Salaam. Hii ni kutokana na kutajwa kwa maeneo ya jiji mfano, Manzese, Tabata, Kiwanda cha Urafiki, Kisutu, Muhimbili nk. Pia ametumia mandhari ya nyumbani mfano nyumbani kwa Mama Ntilie uk.5, mandhari ya hospitali ya Muhimbili uk.89, mandhari ya jaani-jaa la Tabata uk.20.
Kwa hiyo mwandishi ametumia mandhari inayosadifu aliyoyaeleza anaibua dhamira halisi zinazosawiri maisha ya Mtanzania wa leo kwa mandhari hiyo mfano suala la umaskini na wimbi la watoto wa mitaani. 
PATA FULL VIDEO KWA KUBOFYA HAPA