Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Medard Kalemani ameagiza Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuhakikisha mradi wa umeme wa Kinyerezi II unazalisha megawati 30 za umeme nchini ifikapo Desemba mwaka huu. Kalemani amefanya ziara ya kushtukiza katika mradi huo leo asubuhi (Juni 30) ili kujua hali ya utendaji. Amesema taarifa aliyopewa tangu alipowasili ni kuwa mradi huo utazalisha megawati 240 utakapokamilika mwakani ila 30 zikamilike Desemba mwaka huu. "Mradi wa Kinyerezi II tunategemea utupatie megawati 240, lakini lazima tuanze kupata hizo mapema, kwa taarifa niliyosikia tutaanza na megawati 30 sasa niseme megawati hizo tupate ifikikapo Desemba," amesema Kalemani. Amesisitiza kuwa zitakazobakia apewe ratiba za utekelezaji wake ili hadi kufikia Septemba 2017 megawati zote ziwe tayari. Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tanesco, Tito Mwinuka ameomba ushirikiano baina ya Serikali na Shirika hilo ili kufika malengo ya agizo la Naibu Waziri. "Tushirikiane pamoja Tanesco na Serikali kuhakikisha fedha zinapatikana kwa wakati ili kwamba mradi ukamilike kwa wakati," amesema Mwinuka. Kalemani ameongeza kuwa hakutakuwa na uongezaji wa muda katika miradi yote miwili ya Kinyerezi I na II hivyo kuwataka wahusika kufanya kazi kwa nguvu na weledi ili kumaliza kazi. Amesema mradi wa Kinyerezi I umefikia asilimia 35 hali ambayo hairidhishi huku ukitegemewa kutoa megawati 185 kufikia Agosti 2017. "Kufikia Septemba mwakani, tunategemea kuwa na megawati 425 kwa miradi yote miwili bila kupungua, fanyeni kazi sana katika Kinyerezi I," amesema Kalemani. Visit DIDAS BLOG NEWS
0 Comments