Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa ametaka viongozi wa chama hicho kuitisha kikao cha Kamati Kuu ili kujadili namna ya kudhibiti vitendo vya kuwakamata viongozi wa chama hicho vinavyofanywa na wakuu wa mikoa na wilaya. Lowassa ambaye alikuwa waziri mkuu kati ya mwaka 2005 na 2008, alisema hayo juzi wakati wa futari aliyoindaa kwa madiwani na viongozi wa Chadema na wakazi wa Dar es Salaam iliyofanyika Mikocheni. Mwanasiasa huyo alisema hayo wakati viongozi wa Chadema, akiwamo Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye walizuiwa kutembelea miradi ya maendeleo kwa madai kuwa kabla ya ziara hiyo, Meya wa Ubungo, Boniface Jacob alifanya kikao cha chama katika jengo la Serikali. Meya huyo alikamatwa kwa amri ya mkuu wa Wilaya ya Ubungo na kukaa mahabusu kwa saa 48. Mbali na Jacob, Naibu Meya wa Jiji la Arusha, Viola Likindikoki, diwani wa viti maalumu Kata ya Ngarenaro, Happiness Charles na diwani wa viti maalumu Kata ya Olorieni, Sabrina Francis walikamatwa na polisi kwa sababu ambazo hadi sasa hazijawekwa wazi. Calist Lazaro ambaye ni meya wa Jiji la Arusha naye alijikuta akisekwa rumande kwa amri ya mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kwa madai ya kufanya mkusanyiko usio halali wakati akijiandaa kupeleka rambirambi Shule ya Lucky Vincent iliyopoteza wanafunzi 32, walimu wawili na dereva wa gari katika ajali iliyotokea wilayani Karatu. “Hili ni vyema likajadiliwe na kikao na tuwaulize na tuwashirikishe wananchi wetu kwenye uamuzi tutakaouchukua na baada ya hapo tuseme ‘imetosha, na tuchukue hatua’,” alisema. Lowassa alisema ni lazima Kamati Kuu ikutane na kujadaliana kuhusu tabia hiyo aliyoiita ya kubughudhiwa kwa viongozi wa Chadema, hasa wa kuchaguliwa jambo ambalo si jema. Pia, mwanasiasa huyo ambaye alikuwa akivuta hadhira kubwa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, alisema kuzuia mikutano ya hadhara imetosha kwa kuwa wanasiasa wengine, kama Rais John Magufuli wanazunguka sehemu mbalimbali na kuzungumza na wananchi. Alisema mkuu wa wilaya anateuliwa na rais wakati meya wa manispaa anachanguliwa na wananchi, hivyo mwenye wajibu mkubwa wa kuongoza manispaa ni kiongozi anayechaguliwa na wananchi. “Kitendo cha kuwakamata na kuwaweka ndani viongozi wetu si kizuri, ni kuwadhalilisha na hili halijafanyika Ubungo hata Arusha limetokea. Hatuwezi kuruhusu jambo hili likaendelea na likiendelea ni makosa,” alisema. “(Jacob) Nakupa pole ya dhati na masikitiko kwa yaliyokupata juzi,” alisema akigeukiwa kwa meya huyo wa Ubungo. Kuhusu katazo la mikutano ya hadhara, Lowassa alisema wapinzani wananyimwa fursa hiyo lakini akadai upande wa pili wanafanya na kasi yao imezidi kuongezeka. “Rais anazunguka na viongozi wa chama. Pia nimewasikia wanafanya maandamano nchi nzima kumuunga mkono rais. Wao kufanya ni halali sisi ni haramu katika nchi hii na watu walewale, (hiyo) si demokrasia,” alisema. Akipewa nafasi ya kutoa neno la shukrani kwa niaba ya madiwani wenzake, Jacob alielezea kwa kina alivyowekwa mahabusu kwa 48, akisema alikuwa na hasira, lakini busara zilimuongoza na kuamua kumsamehe mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kisare Makori kwa sababu tatu. “Sababu ya kwanza nimepokea pole na masikitiko yake wakati nikiwa mahabusu; pili hakuwa na namna na siyo kosa lake. Najua kuna mtu alimtuma kufanya hivyo na kama asingefanya kibarua chake kingekuwa mashakani,” alisema. “Tatu ni muungwana na ninaahidi kufanya naye kazi bega kwa bega, ila naomba mtambue taarifa nilizozipata ni kwamba DC alipata maagizo na sina haja ya kumtaja hapa,” alisema Jacob. Meya huyo alisema ana taarifa nyingine kwamba kazi ya kumkamata na kumuweka mahabusu ilitakiwa ifanyike siku nyingi, lakini alikuwa makini. Alisema kuna watu wana lengo la kumrudisha nyuma kutokana na kazi nzuri anayoifanya. Pia, alisema hana sababu ya kumlaani wala kumtenga Makori kwa kuwa alipewa amri na kwamba haikuwa kosa kwake kufanya mkutano na viongozi wa Chadema katika ukumbi wa halmashauri. “Nikiwa diwani wa Manispaa ya Kinondoni nilibahatika kupata kalenda tano ambazo zipo nyumbani kwangu na baadhi ya picha zilizomo katika kalenda hizo zinaonyesha meya na viongozi wa CCM wakikagua miradi mbalimbali ikiwamo ya shule na madaraja,” alisema Jacob. Alisema tatizo ni kuonekana kwa Sumaye katika eneo hilo, hali ambayo ingewapa wakati mgumu viongozi wa wilaya hiyo ambao wangeshindwa kuwaeleza wakubwa wao. “Mimi ni shujaa na ngangari katika masuala ya mahabusu. Ile mahabusu ya saa 48 ilikuwa soft (laini) kwangu. Katika safari yangu ya kisiasa nimekaa jela mara nne na mahabusu 16, ikiwamo ya Stakishari ila ya Mbezi sikuwahi kukaa kwa sababu ni mpya,” alisema na kuongeza kuwa: “Msinipe pole nipeni hongera na kituo hiki cha polisi wa Mbezi nimeahidi kukipelekea rangi na vifaa vya usafi kwa ukarabati zaidi,” alisema Jacob ambaye ni diwani wa Ubungo (Chadema). Hata hivyo, Jacob aliungana na Lowassa kuhusu kuitishwa kwa kikao cha Kamati Kuu na kuwaeleza Watanzania kwamba yeye atakuwa mwanasiasa wa mwisho kuwekwa ndani kwa amri ya wakuu wa mikoa na wilaya. Alisema atahakikisha anaipingania kwa nguvu zote ikiwamo kisheria amri ya wakuu wa mikoa na wilaya ya kuwaweka ndani baadhi ya watu wakiwamo viongozi wa upinzani kwani jambo hilo likiachwa litawaathiri wananchi wengine. Visit DIDAS BLOG NEWS
0 Comments